Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nguvu ya kijeshi kutumika dhidi ya waasi wa FDLR: UM

Nguvu ya kijeshi kutumika dhidi ya waasi wa FDLR: UM

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, siku chache baada ya mwisho wa kipindi cha miezi sita kilichotolewa kwa waasi wa FDLR  kujisalimisha kwa amani, Umoja wa Mataifa umesema nguvu ya kijeshi itatumika.

Akizungumza na radio Okapi Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC Jenerali Abdallah Wafy, amesema hatua hiyo inafuatia FDLR kushindwa kutumia fursa hii ya kihistoria ya kujisalimisha kwa njia ya amani.

(SAUTI YA WAFY)

Leo, kila mtu anakubali kwamba hakuna suluhu nyingine bali ya kijeshi. Sasa suluhu ya kijeshi itatekelezwa ili kusalimisha FDLR kwa nguvu. Tumejiandaa pamoja na jeshi la kitaifa la Congo, FARDC, ili utaritibu huu ufanyike kwa kuheshimu masharti na sheria ya kibinadamu, bila, kuathiri watu wa kawaida nasisitiza hilo. 

Kundi la waasi wa FDLR linatishia usalama wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa zaidi ya miaka kumi na tano. Taasisi za kikanda ikiwemo mkutano wa kimataifa wa maziwa makuu, ICGLR na muungano wa nchi za kusini mwa Afrika, SADC, ziliwapa miezi sita ili wajisalimishe kamili na bila masharti na warejeshwe nchini Rwanda.