Ufadhili wawezesha WFP kurejesha mgao wa chakula kwa wakimbizi Kenya

30 Disemba 2014

Shirika la chakula duniani WFP limetangaza kurejelea mgao wa chakula kwa wakimbizi walioko nchini Kenya mwezi Januari kufuatia ufadhili kutoka kwa wahisani. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

WFP hugawa chakula mara mbili kwa mwezi kwa takriban wakimbizi laki tano katika kambi za Dadaab na Kakuma zilizoko kaskazini mwa Kenya. Ukosefu wa fedha ulipelekea shirika hilo kupunguza mgao wa chakula kwa nusu.

WFP kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR walizindua ombi la fedha mwezi Oktoba. Kufikia sasa kupitia wadau, serikali na shirika hilo limechangisha dola milioni 45 na kuwezesha kurejelea shughuli za kutoa msaada.

Challis McDonough ni msemaji wa WFP mjini Nairobi Kenya.

(Sauti ya Challis)

“Tunawashukuru sana wahisani ambao waliitikia ombi na kutuwezesha kurejesha mgao wa chakula kwa asilimia 100 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wakimbizi. Mwezi Oktoba tulikuwa na chakula kidogo tu cha hadi mwisho wa mwaka na ili kuweza kuendelea kutoa mgao wa chakula ilitulazimu kupunguza kiwango cha mgao.”

Sera ya serikali ya Kenya haiwaruhusu wakimbizi kufanya kazi nje ya kambi, kwa hiyo wanategemea kwa pakubwa msaada wa kimataifa. Kila mwezi WFP hutoa mgao wa tani 9700 kwa wakimbizi laki tano walioko Kenya kwa gharama ya takriban dola milioni 10.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter