Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulio katika vituo vya mafuta na uhalifu mwingine hauna tija kwa Libya: UNSMIL

Mji wa Sirte, nchini Libya, baada ya mapigano ya 2011. Picha ya IRIN/Heba Aly

Mashambulio katika vituo vya mafuta na uhalifu mwingine hauna tija kwa Libya: UNSMIL

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umelaani vikali mashambulio mapya katika meneo ya mitambo ya mafuta  ambapo matenki ya hifadhi yake yaliripotiwa kuchomwa moto katika kituo kikuu cha mafuta cha Sidra. Ujumbe umetaka kusitishwa kwa mashambulizi hayo haraka.

Taarifa ya UNSMIL inaonya juu ya madhara ya kiuchumi na mazingira kutokana na ukatili na uharibifu wa maeneo ya mafuta na kutaka vikosi nchini humo kushirikiana ili kuruhusu wafanyakazi wa zima moto kuuzima moto huo. Ujumbe pia umerejela wito wake wa usitishwaji wa uhasama ikiwamo mashambulizi ya anga yamayotishia kukua kwa mgogoro.

Kwa mujibu wa UNSMIL  mashambulio ni ukiukwaji wa maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Libya . Ujumbe umeongeza kuwa mafuta ni mali ya Walibya wote katika uhai wa uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine UNSMIL umelaani shambulio la Desemba 25 lililotekelezwa na watu wasiofahamika waliojihami katika kituo cha umeme mjini Sirte na kusababisha vifo vya walinzi kadhaa .

Ujumbe umetaka viongozi wenye ushawishi nchini Libya  kukomesha mfululizo wa uhalifu uliouita usio na maana na kusisitiza kuwa hakuna mshindi katika mgogoro huo . UNSMIL pia umesema maeneo yenye mafuta na mgogoro wake unakwamisha juhudi zinazondelea za kuitisha majadiliano ya kisiasa.