Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola ni hatari kwa wananchi wote wa Guinea: Ban

Wahudumu wa afya wakihakikisha wamevaa vizuri vifaa vya kujikinga kabla ya kuanza kutoa huduma ya tiba dhidi ya Ebola. (Picha:Worldbank)

Ebola ni hatari kwa wananchi wote wa Guinea: Ban

Mshikamano wa pamoja ni muhimu zaidi hivi sasa na ndio utawezesha kutokomeza Ebola, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alipozungumza na waandishi wa habari mjini Conakry, Guinea.

Ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kujionea hali halisi ya Ebola Afrika Magharibi na kuonyesha mshikamano dhidi ya mlipuko, Ban amesema mshikamano baina ya serikali ya Guinea, wadau na wananchi utasaidia kumaliza mlipuko wa Ebola ambao kuenea kwake ni hatari kwa kila mkazi wa nchi hiyo.

Katibu Mkuu amesema amezungumza na Rais Alpha Conde wa Guinea kuhusu hofu ya kuenea kwa mlipuko maeneo ya Forest Guinea ambako wamekubaliana kuwa ushirikiano kupitia ushirikiano wa Mano River utawezesha kudhibiti mlipuko usivuke mipaka na kuingia nchi jirani.

Ban amesema wakati harakati dhidi ya Ebola zinaendelea, Umoja wa Mataifa na wadau unaangalia pia harakati za kujikwamua baada ya mlipuko akiwahakikishia kuwa Umoja wa Mataia utaendelea kuwa nao.

Tayari ameshatembelea Sierra Leone na Liberia na pia atakwenda Mali kuonyesha mshikamano wakati huu ambapo Ebola imeshasababisha vifo vya watu zaidi ya 6800 lakini kasi ya kuenea kwake inapungua baadhi ya maeneo.