Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yatumia msimu wa ukame kusafirisha chakula cha msaada Sudan Kusini

UN Photo/Martine Perret
Msaada wa chakula nchini Sudan Kusini.

WFP yatumia msimu wa ukame kusafirisha chakula cha msaada Sudan Kusini

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limeanza operesheni ya kupeleka chakula nchini Sudan kusini wakati huu ambapo msimu wa ukame umeanza na barabara zinapitika kwa urahisi.

Msemaji wa WFP Elizabeth Byrs amesema lengo la mpango huo ni kuepusha baa la njaa kwa watu zaidi ya Milioni 2.5 ambao wataanza mwaka mpya bila kufahamu watakula nini.

Bi. Byrs amesema utapiamlo nchini Sudan Kusini uko katika kiwango cha juu na wanahitaji dola Milioni 341 kukidhi mahitaji ya chakula kwa miezi sita ijayo.

Hata hivyo WFP inasema  inasema janga la njaa Sudan Kusini linasababishwa na mapigano na hiyo imetoa wito kwa vikundi vinavyokinzana kuweka silaha chini ili msaada wa chakula ufikie walengwa kwa wakati.

Zaidi ya watu Milioni 1.9 wamekimbia makazi yao Sudan Kusini tangu mapigano yaanze nchini humo mwezi Disemba mwaka jana kati ya serikali an vikosi vya waasi.