Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS imelaani mashambulizi yanayowalenga raia, Bentiu

Maelfu ya wakimbizi hukimbilia vituo vya UNMISS kwa uhifadhi ili kuepuka mzozo.(Picha ya UM/JC McIlwaine)

UNMISS imelaani mashambulizi yanayowalenga raia, Bentiu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS kupitia kitengo chake cha haki za binadamu umetoa ripoti inayoelezea madai ya vikosi vya upinzani kuwaua takriban raia 11 na ukatili dhidi ya binadamu wakati wa mashambulizi katika mji mkuu wa jimbo la Unity, Bentiu mwezi Oktoba.

Wataalam wa haki za binadamu wa UNMISS wamepokea taarifa kutoka vyanzo mbali mbali na madai ya vikosi vya waasi kuwateka na kuwabaka wakaazi wanawake wa Bentiu baada ya vikosi vya serikali kuondoka Bentiu jioni ya Oktoba 29 mwaka huu.

Ripoti hiyo ina majina ya wanawake 14 ambao wanadaiwa kutekwa na vikundi vya waasi wakati wa saa tano walizoteka mji wa Bentiu.

Kulingana na ripoti mashahidi walishuhudia wanawake wawili na mtoto wa miezi sita wakiuawa nyumbani kwao katika eneo la Dere huko Bentiu.

UNMISS imesema kwamba vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinafanyika mara kwa mara na vinahusisha pande mbili katika mzozo.

Utafiti wa hivi sasa umebainisha kwamba vikosi vya upinzani vilikiuka haki za bindamu ambavyo ni ukiukaji wa haki za kimataifa na huenda ikawa ukatili wa kivita.