Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuko nanyi hadi Ebola itokomezwe; Ban awaeleza waliberia

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon akinawa mikono baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Roberts, kwenye mji mkuu wa Liberia, Monrovia. (Picha:UNMIL-Facebook)

Tuko nanyi hadi Ebola itokomezwe; Ban awaeleza waliberia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ambaye yuko Afrika Magharibi kujionea hali halisi ya udhibiti wa mlipuko wa Ebola na kuonyesha mshikamano na wananchi na serikali, amesifu jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo ambao hadi sasa umeua zaidi ya watu 6800. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Baada ya kufanya ziara na kukutana na wadau wanaoongoza harakati dhidi ya Ebola nchini Liberia, Ban ambaye ameongozana na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani Dkt. Margaret Chan amewaambia waandishi wa habari kuwa mshikamano wa dunia dhidi ya Ebola umepunguza kasi ya kuenea kwa Ebola nchini humo, akipongeza wananchi huku akitoa hakikisho.

(Sauti Ban)

“Tumeazimia kuwa nanyi mnapokabiliana na kitisho hiki kikubwa, na tutakuwa nanyi hadi mlipuko utakapotokomezwa na nchi kuibuka. Leo tuna sababu ya kuwa na  matumaini kiasi kuwa mlipuko huu mkubwa utatokomezwa kwani kasi ya kuenea kwa kirusi Liberia inapungua. Zaidi ya yote hii inatokana na wananchi wenyewe walivyojitoa kwa dhati, mkakati wetu wa kudhibiti Ebola unafanya kazi.”

Hata hivyo amesema kuna changamoto ya rasilimali watu, vifaa na fedha lakini muhimu ni wananchi kubadili tamaduni zinazoweza kukwamisha juhudi, lakini pia amezungumzia uchaguzi wa maseneta siku ya Jumamosi.

(Sauti Ban)

“Uchaguzi huu ni fursa kwa Liberia na wananchi wake kudhihirishia ulimwengu ni wapi imetoka. Nasihi wananchi wote wahakikishe  uchaguzi unakuwa wa amani na haki. Halikadhalika fuateni miongozo ya afya dhidi ya Ebola ili mjikinge ninyi na wapendwa wenu”.

Kwa upande wake Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia ametoa shukrani kwa jamii ya kimataifa kwa kasi ya usaidizi akisema awali ilikuwa taratibu lakini sasa inaridhisha na matunda yanaonekana.