Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghala la vifaa tiba dhidi ya Ebola lateketea kwa moto, UNMEER yazungumza

Mkuu wa UNMEER Anthony Banbury. (Picha:UN/Eskinder Debebe)

Ghala la vifaa tiba dhidi ya Ebola lateketea kwa moto, UNMEER yazungumza

Ghala lililokuwa na vifaa tiba dhidi ya Ebola limeteketea kwa moto huko Conakry mji mkuu wa Guinea ambapo ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia dharura ya Ebola, UNMEER umesema ni hasara kubwa lakini haitarejesha nyuma operesheni dhidi ya ugonjwa huo.

Miongoni mwa vifaa vilivyokuwa vimehifadhiwa ndani ya bohari hiyo inayotumiwa na Shirika la afya duniani WHO na wadau wake ni pamoja na madawa na vifaa vya maabara na linasimamiwa na UNMEER.

Mkuu wa UNMEER Anthony Banbury amesema hasara waliyopata ni ya kusikitisha lakini muhimu ni kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa na wanachofanya sasa ni kuweka vifaa tiba vingine ili harakati dhidi ya Ebola ziendelee.

Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na hadi sasa hasara kamili iliyopatikana haijafahamika.

Guinea ni moja ya nchi tatu za Afrika Magharibi zilizokumbwa zaidi na mlipuko wa Ebola.

Hadi sasa Ebola imesababisha vifo vya watu 6,841 kati ya visa 18,464 vilivyothitibishwa hadi sasa huko Guinea, Liberia na Sierra Leone.