CERF yapata ahadi ya zaidi ya dola Milioni 418 kwa mwaka 2015.

17 Disemba 2014

Jijini New York, Marekani wahisani wameahidi zaidi ya dola 418 kwa ajili ya mfuko mkuu wa dharura wa majanga wa Umoja wa Mataifa, CERF utakaowezesha shughuli za usaidizi wa kibinadamu kwa mwaka 2015.

Ahadi hizo zimetolewa wakati wa mkutano wa mwaka wa ngazi ya juu ambapo Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na uratibu wa misaada ya kibinadamu Valerie Amos amesema yatia moyo kuona wahisani wanajitolea licha ya mazingira magumu ya kiuchumi duniani.

Wahisani kadhaa waliongeza michango yao ikiwemo Ubelgiji, Irelandi, Uholanzi, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo Bi. Amos amesema katika miaka minne ya jukumu lake ameshuhudia vile ambavyo mfuko huo unabadili maisha miongoni mwa wahitaji.

Ametolea mfano nchini Mali, Sudan Kusini, Haiti na Afghanistan.

Tangu mwaka 2006 wanachama 125 wa Umoja wa Mataifa na nchi zenye hadhi ya uangalizi pamoja na mamlaka za kikanda, taasisi, watu binafsi na wahisani wamechangia zaidi ya dola bilioni 3.7 kwa mfuko wa CERF.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter