Hataza na alama za biashara, China yaongoza:WIPO

16 Disemba 2014

China inazidi kushika kasi duniani katika umiliki wa hataza na hivyo kubadili mwelekeo kutoka bidhaa zinazotengenezwa China hadi bidhaa zilizobuniwa China.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Jumanne na shirika la hakimiliki duniani, WIPO ikieleza kuwa China na kwa kiasi kidogo Marekani zinasalia kuongoza katika ubunifu wa bidhaa.

WIPO inasema matokeo ya ripoti hiyo ni muhimu kwa kuwa yanaakisi hali ya uchumi wa zaidi ya mataifa 100.

Matokeo ya ripoti hiyo yalizingatia maombi ya haki ya hataza na alama za biashara yaliyowasilishwa na nchi mbali mbali ambapo China iliongoza kwa kuwa na Theluthi Mbili ya maombi zaidi ya Milioni Mbili na Nusu ya hataza yaliyowalishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa WIPO Francis Gurry anasema kiwango hicho ni kiashiria cha pengo la ukuaji uchumi kati ya China na kwingineko.

(Sauti ya Francis)

 Kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo linachochewa na China. Imewasilisha mambo mengi ya umiliki wa Hataza na alama za biashara. Kwa mantiki hiyo mwelekeo ni kuhama kutoka iliyotengenezwa China hadi iliyobuniwa China.”

WIPO imesema kiwango cha uwekezaji wa China kwenye Utafiti na Maendeleo ni cha pili baada ya Marekani na kuna uwezakano kiwango hicho kikalingana ifikapo mwaka 2019.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud