Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu dhidi ya Luteni Kanali Engangela ni ushindi: MONUSCO

Usalama wa mtoto kama huku unawekwa mashakani na watendaji wa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu. (Picha:MONUSCO/Abel Kavanagh)

Hukumu dhidi ya Luteni Kanali Engangela ni ushindi: MONUSCO

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO umekaribisha hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya Luteni Kanali Bedi Engangela aliyepatikana na hatia ya uhalifu dhidi ya kibinamu.

Imeelezwa kuwa Engangela al maarufu Kanali 106 amehukumiwa kwa makosa ya ubakaji, utumikishaji, utesaji aliyotenda huko jimbo la Kivu Kusini kati ya mwaka 2005 na 2007.

Kaimu Mkurugenzi wa ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini DRC Abdoul Aziz Thioye amepongeza mamlaka za nchi hiyo kwa jitihada zake za kuhakikisha hadi inatendeka dhidi ya Engangela na kwamba hukumu hiyo ni ujumbe tosha kwa watekelezaji wa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu.

Hukumu ya leo imefikiwa baada ya miaka Saba ya jitihada za mamlaka za sheria DRC kwa uasidizi wa MONUSCO, UNDP na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali za kuhakikisha hakuna ukwepaji sheria kwa makosa ya aina hiyo.

Mwezi uliopita, afisa mwandamizi wa jeshi la serikali FARDC Jenerali Jérôme Kakwavu alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa makosa ya uhalifu wa kivita.