Mauaji ya watoto wa shule Pakistani, UM walaani vikali

16 Disemba 2014

Umoja wa Mataifa umelaani vikali mauaji ya kikatili ya zaidi ya watoto 130 kwenye shule moja huko Peshawar nchini Paksitani ukitaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu Ban Ki-Moon kabla ya kuzungumza kwenye mkutano wa baraza la Usalama amesema tukio hilo ni la kulaaniwa vikali akituma rambi rambi kwa wananchi na serikali ya Pakistani akisema shule ni mahali pa amani…

(Sauti ya Ban)

“Hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha ukatili huo. Hakuna kero yoyote inayoweza kuhalalisha kitendo hicho. Ni kitendo cha kutisha kinachoashiria woga kushambulia watoto wasioweza kujilinda. Shule zinapaswa kuwa salama na kutoa fursa ya kusoma. Kupata elimu ni haki ya kila mtoto. Kwenda shule haipaswi kuwa jambo la kijasiri.”

Nchini Paksitani, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Timo Pakkala amesema tukio hilo la Jumanne limeleta machungu kwa wapakistani na kwamba kushambulia watoto walioko shuleni ni kinyume na misingi ya kulinda utu wa binadamu.

Naye Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein amesema tukio hilo halipaswi kuvumiliwa na watu wote washikamane kupinga matukio ya aina hiyo.

Kwa upande wake UNICEF imetaka kila mtu kusaidia wazazi wa Pakistani ambao wanataka watoto wao wapate elimu, sambamba na wale wanaotoa elimu hiyo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud