Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maeneo athirika Peru yasipatiwe wawekezaji wa mafuta: Wataalamu

UN Photo/Joseane Daher
Picha:

Maeneo athirika Peru yasipatiwe wawekezaji wa mafuta: Wataalamu

Watalamu wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa hatua yoyote ya utoaji upya wa leseni kwa maeneo yaliyoharibiwa vibaya kimazingira nchini Peru kunaweza kuchochea isivyo kifani vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu.

Wataalamu hao wamesema kuwa iwapo hatua hiyo itatekelezwa basi waathirika wakubwa watakuwa wakazi asilia wa jimbo la Loreta ambao wanaweza wakijikuta wakitaabika kiafya, chakula na maji.

Onyo la wataalamu hao limekuja huku Serikali ya Peru ikiwa imepitisha uamuzi wa kutoa upya leseni kwa kampuni za mafuta kuendelea na shughuli zake kwenye eneo hilo.

Hivi karibuni kampuni ya uzalishaji mafuta inayomilikiwa na Serikali iliweka saini ya makubaliano na wakazi wa eneo hilo kwa ajili ya kukarabati upya maeneo yote ambayo yalikuwa yameharibiwa vibaya kutokana na shughuli za mafuta.