Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC, M23 tekelezeni vipengele vyote vya makubaliano

Hili ni lori lililokuwa limebeba silaha za kundi la M23.(Picha ya UM/Sylvain Liechti)

DRC, M23 tekelezeni vipengele vyote vya makubaliano

Umoja wa Mataifa umezitaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kundi la waasi wa M23 kutekeleza bila kuacha sehemu makubaliano yaliyotiwa saini mwaka mmoja nyuma mjini Nairobi nchini Kenya yaliyofungua mlango wa kumalizika kwa mapigano. Taarifa kamili na George Njogopa.

(Taarifa ya George)

Pande hizo ambazo ziliiingia kwenye mapigano kwa muda mrefu zilitiliana saini makubaliano ya amani chini ya upatanishi wa Rais Yowei Mseveni wa Uganda na  kukaribisha enzi mpya iliyosaidia kupatikana kwa amani.

Wakizungumzia kuhusu makubaliano hayo wakati huu kunapotimia mwaka mmoja tangu kusainiwa kwake, maofisa wa UN akiwamo Mwakilishi wa Katibu Mkuu katika eneo la Maziwa Makuu Said Djinnit, na Mkuu wa Vikosi vya kimataifa  MONUSCO Martin Kobler wamesisitiza haja ya kutekeleza vipengele vyote vilivyomo kwenye maafikiano hayo.

Miongoni mwa maeneo yaliyotajwa kwenye mkataba huo wa usitishwaji wa mapigano ni pamoja na kwa pande zote kuweka chini silaha na ujenzi wa Kongo mpya.

Maofisa hao wa UN wamepongeza hatua zinazochukuliwa na pande zote ikiwamo kwa serikali ya Kongo ambayo imekubali kutoa msamaha kwa wapiganaji wa M23 na kuwarejesha nyumbani wapiganaji wengine walioko huko Uganda na Rwanda.