Utumaji fedha kutoka ughaibuni kuongezeka: ILO

12 Disemba 2014

Shirika la kazi duniani, ILO limesema elimu ya matumizi ya fedha ni muhimu kwa wahamiaji wanaoishi ughaibuni ili fedha wanazopata ziweze siyo tu kunafaisha wao bali pia familia zao ambako wanatuma fedha hizo.

ILO imesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kiwango kikubwa cha fedha kinachotumwa kikitolea mfano kuwa mwishoni mwa mwaka huu jumla ya dola Bilioni 436 zitakuwa zimetumwa na wahamiaji kwenda kwenye familia zao.

Kiwango hicho kitafikia dola Bilioni 540 mwishoni mwa mwaka 2016.

Nchini Ufaransa ILO inaunga mkono mradi wa elimu ya matumizi ya fedha kwa wafanyakazi wahamiaji, FORIM ambapo afisa kutoka ILO Séverine Deboos amesema elimu hiyo itasaidia siyo tu matumizi yao bali pia utunzaji iwapo watarejea nyumbani baada ya maisha ya ughaibuni.

Bi. Deboos amesema wafanyakazi wahamiaji wanapaswa kuwa na uelewa wa lini na wakati gani kuchukua mkopo, jinsi ya kuweka akiba na hata mambo ya kuzingatia wakati wanapoingia mkataba unaohusiana na masuala ya fedha.

Mradi aina ya FORIM unatekelezwa nchi kadhaa ikiwemo Ethiopia, Indonesia, Kenya na Mali.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud