Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati dhidi ya Ebola, UNICEF kuhitaji dola Milioni 500 hadi Juni mwakani

Juhudi za kutoa elimu kwa watoto kwa ajili ya kukabiliana na Ebola nchini Liberia.(c) UNICEF / Liberia / 2014 / Carolyn Marie Kindelan

Harakati dhidi ya Ebola, UNICEF kuhitaji dola Milioni 500 hadi Juni mwakani

Katika harakati za kukabiliana na Ebola, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema litahitaji dola Milioni 500 hadi mwezi Juni mwakani ili kuimarisha ustawi wa watoto kwenye maeneo ya mlipuko.

Msemaji wa UNICEF huko Geneva, Sarah Crowe amesema maeneo husika ni Guinea, Sierra Leone na Liberia akieleza kuwa matumizi ya fedha ni pamoja na kujenga maeneo ya kutenga wagonjwa, na kuunganisha watoto 10,000 na jamaa zao baada ya wazazi wao kufariki dunia kutokana na Ebola.

Halikadhalika watatoa mafunzo kwa wafanyakazi 60,000 wa kujitolea ambao wataendesha kampeni ya nyumba kwa nyumba.

(Sauti ya Sarah)

“Tunajua si rahisi kujitoa kwenye mlipuko huu na ushiriki wa jamii ni muhimu sana na ndio maana tunasaidia vituo 300 vya kijamii vya kutoa huduma. Lengo ni kuhakikisha wanabadili tabia na inachukua muda kubadili tabia, kuongeza uelewa na kubadili mtazamo na hatimaye kubadili tabia. Lakini mwelekeo unatia moyo.”

Tayari UNICEF imepokea dola Milioni 200 kati ya kiwango inachohitaji.