Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwamko wa wananchi dhidi ya Ebola bado unahitajika: Dkt. Nabarro

Mjumbe maalum wa UM kuhusu Ebola Dkt. David Nabarro akiangalia harakati za upimaji joto la mwili alipotembelea Guinea hivi karibuni. (Picha:UN/Simon Ruf)

Mwamko wa wananchi dhidi ya Ebola bado unahitajika: Dkt. Nabarro

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, Dkt.David Nabarro amesema ametiwa moyo na mabadiliko makubwa yaliyopatikana kwenye harakati dhidi ya ugonjwa huo huko Liberia, Mali, Sierra Leone na Guinea.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, kufuatia ziara yake hivi karibuni nchini humo, Dkt. Nabarro amesema ameshuhudia mabadiliko makubwa wakati wa ziara yake hivi karibuni kwenye nchi hizo akilinganisha na mwezi Septemba, akisema hali imeimarika kwa upande wa ubora na wigo wa huduma dhidi ya Ebola.

Amesema ipo tofauti ya idadi ya wagonjwa katika maeneo mathalani mijini, mipakani na maeneo yaliyo ndani zaidi lakini kwa ujumla idadi ya wagonjwa wapya inapungua hasa kwenye maeneo ambako jamii ina mwamko dhidi ya Ebola mathalani Mashariki mwa Sierra Leone.

Hata hivyo amesema bado kuna maeneo ambako jamii haina mwamko..

 (Sauti ya Dkt. Nabarro)

"Lakini katika baadhi ya maeneo bado kuna vitisho na hivyo mara nyingi inalazimu kuwepo kwa mashauriano kati ya watoa huduma na jamii ili kuweza kuingia na kufanya nao kazi. Bila ya mashauriano hayo kunaweza kuwepo kwa matatizo na machungu ambayo wakati mwingine yanaweza kusababisha mvutano.”

Amesema harakati dhidi ya Ebola zitaendelea kwa miezi kadhaa lakini mwelekeo unatia moyo.