Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utesaji wa wafungwa; Marekani yaendelea kulaumiwa kila kona

UN Photo - Jean-Marc Ferre
Juan E Mendez.

Utesaji wa wafungwa; Marekani yaendelea kulaumiwa kila kona

Marekani imeendelea kutupiwa lawama kutokana na kitendo chake cha kukacha kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuwawajibisha baadhi ya askari waliobainika kukiuka haki za binadamu kwa kuendesha vitendo vya mateso kwa watuhumiwa.Taarifa kamili na George Njogopa(Taarifa ya George)

Kulingana na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na utesaji  Juan Mendez kushindwa kuwawajibisha wale waliohusika kwenye vitendo hivyo kunaweza kusabibisha pia mataifa mengine kufuata mkondo wa aina hiyo jambo ambalo amesisitiza kuwa siyo mujarabu kwa kulinda haki za binadamu.

Mtaalamu huyo ametoa tahadhari hiyo ikiwa ni siku moja tu baada ya ripoti iliyotolewa na kamati ya usalama ya Seneti kuwatuhumu maofisa wa shirika la ujasusi la Marekani kwa ukiukwaji wa haki za binadamu kutokana na mwenendo wake wa kuwatesa watuhumiwa.

Ripoti hiyi imesema kuwa mara nyingine maofisa wa CIA waliendesha upelelezi katika mazingira ya kikatilii na wakati mwingine waliwatesa vibaya watuhumiwa ambao walihisishwa na  shambulizi la Septemba 11 mjini New York.

Akifafanua zaidi Mendez pamoja na kuipongeza kamati ya Senete kwa kufichua ukweli wa mambo aliitaka Marekani kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba vitendo vya namna hiyo havijirudii tena.