Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo mpya wa ununuzi wa dawa za HIV kuokoa dola Milioni 100

Picha@UNAIDS

Mfumo mpya wa ununuzi wa dawa za HIV kuokoa dola Milioni 100

Mfuko wa dunia unaofadhili vita dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria unaandaa makubaliano mapya ya ununuzi wa dawa dhidi ya Ukimwi utakaookoa dola Milioni 100 ndani ya miaka miwili. Kupitia mfumo huo mpya, mfuko huo utaingia makubaliano na wasambazaji wanane, hali ambayo itawezesha upatikanaji wa dawa dhidi ya HIV kuwa wa uhakika zaidi, bei itakuwa nafuu na hata usambazaji wake utakuwa ni rahisi na kwa muda mrefu.

Halikadhalika kutakuwa na uwazi na kupunguza hatari na gharama kwa nchi ambazo zinatekeleza mipango ya kupatia tiba watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Afisa manunuzi wa mfuko huo Christopher Game amesema fedha hizo zitakazookolewa kupitia mfumo huo mpya wa ununuzi, zinaweza kuwekezwa kwenye dawa na mipango mingine ya kuokoa maisha ya watu.

Hadi mwaka huu wa 2014, mfuko huo umekuwa ukitoa misaada ya fedha kwa mipango inayowezessha watu Milioni 7.3 wanaoishi HIV kupata tiba dhidi ya magonjwa nyemelezi, kiwango ambacho ni ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka jana.