Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na viongozi mbali mbali huko Peru kando ya COP20

Katibu Mkuu Ban Ki-moon wakati alipokutana na waziri wa maji na mazingira kutoka Afrika Kusini Edna Molewa.(Picha ya UM/Mark Garten)

Ban akutana na viongozi mbali mbali huko Peru kando ya COP20

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo na viongozi mbali mbali kando mwa mkutano wa 20 wa mabadiliko ya tabianchi, COP20 huko Lima, Peru.Miongoni mwao ni Waziri wa Mazingira wa Afrika Kusini, Edna Molewa, ambapo Ban amekaribisha taarifa ya kwamba nchi hiyo itakuwa mwenyekiti wa kundi la 77 na China mwaka 2015.

Ametoa wito kwa Afrika Kusini kuendelea na mchango wake adhimu kwenye mikataba ya kimataifa huku akiangazia zaidi dhima ongozi ya Taifa hilo katika kushirikiana na nchi zinazoendelea na zile zilizoendelea miezi kabla ya mkutano ujao wa COP21 huko Paris Ufaransa.

Wakati huo huo Ban amekuwa na mazungumzo na Waziri wa Mazingira wa Japan Yoshio Mochizuki, ambapo amesifu uongozi wa nchi hiyo kwenye mfuko wa mabadiliko ya Tabianchi.

Ban amesema ni matumaini yake kuwa ahadi ya Japan kwenye mfuko huo pamoja na ile ya Marekani itatoa changamoto kwa mataifa mengine kuchukua hatua kama hizo.