Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waafrika tumetupa minyororo ya mwili bado ya kifikra:Kutesa

Minyororo iliyokuwa ikitumika kuwafunga wafungwa wakati wa biashara ya utumwa ya Atlantiki(Picha ya UM/Mark Garten

Waafrika tumetupa minyororo ya mwili bado ya kifikra:Kutesa

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa amesema harakati za kuondokana na madhila ya utumwa na ukoloni ziende sambamba na zile za kuondokana na utumwa wa kifikra.Kutesa amesema hayo wakati wa uzinduzi wa muongo wa watu wenye asili ya Afrika 2015-2024 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa wenye lengo la kuendeleza heshima,  ulinzi na uhuru wa kundi hilo kwa mujibu wa tamko la haki za binadamu.

(Sauti ya Kutesa)

“Wakati tunakumbuka kujikwamua kutoka utumwani, nadhani wakazi wa Afrika na wale wenye asili ya bara hilo wanakabiliwa na changamoto moja leo hii, na hiyo ni kuondokana na utumwa wa kifikra. Changamoto hiyo ni lazima tukabiliane nayo nyumbani Afrika na ughaibuni la sivyo tutaendelea kuwa kwenye minyororo ya utumwa.”

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulisomwa kwa niaba yake na Msaidizi wake wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu Valerie Amos. Ujumbe pamoja na kutaja  ukoloni na utumwa kuwa chanzo cha madhila yanayoendelea kukumba watu wenye asili ya Afrika, ulitoa pia pendekezo.

(Sauti ya Amos)

“Sote tunapaswa kuchukua hatua zaidi kuhakikisha haki kwenye mfumo wa kusimamia sheria na kuzingatia na kuendeleza haki za binadamu za watu wenye asili ya Afrika popote pale duniani.”