Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti za Marekani na Brazil ni kiashiria utesaji bado upo: Kamishna Zeid

Picha: OHCHR

Ripoti za Marekani na Brazil ni kiashiria utesaji bado upo: Kamishna Zeid

Ikiwa ni miaka 30 tangu kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa dhidi ya Mateso, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein amesihi mataifa kukomesha mateso.

Katika ujumbe wake Kamishna Zeid amesema siku ya leo siyo tu ya kuadhimisha kuridhiwa kwa tamko la haki za binadamu bali pia mkataba dhidi ya Mateso akitumia fursa hiyo kugusia ripoti ya baraza la seneti la Marekani kuhusu upelelezi na mateso ya watuhumiwa wa ugaidi iliyochapishwa Jumanne.

Amesema ripoti hiyo ni kiashiria kuwa bado mateso yanaendelea katika baadhi ya nchi 156 zilizoridhia Mkataba dhidi ya mateso na licha ya kuwepo kwa sheria zinazoharamisha utesaji.

Kamishna Zeid amesema uthibitisho dhahiri kuwa taifa kama Marekani bado linatesa watu kwa kiwango hicho hadi hivi karibuni ni kumbusho kwamba dunia yahitaji juhudi zaidi kutokomeza mateso popote pale.

Halikadhalika, Kamishna Zeid amekaribisha kutolewa kwa repoti ya Tume ya Kitaifa ya Ukweli ya Brazil inayoonyesha matumizi makubwa ya mateso na ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa wakati wa utawala wa kijeshi kuanzia mwaka 1964 hadi 1985.