Mtaalamu wa UM atoa wito kushtakiwa kwa CIA na viongozi wengine wa Marekani.

9 Disemba 2014

Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kupambana na ugaidi na haki za binadamu, Ben Emmerson ameunga mkono muhtasari wa ripoti ya Kamati teule ya baraza la seneti la Marekani kuhusu  mateso na kupotea kwa watuhumiwa wa ugaidi kulikofanywa na shirika la kijasusi la Marekani, CIA wakati wa utawala wa George W. Bush.

Bwana Emerson katika taarifa amesema imechukua miaka minne tangu ripoti hiyo kukamilika na amesifu utawala wa sasa wa Marekani kwa kupinga shinikizo la ndani la kuficha matokeo hayo aliyosema ni muhimu.

Mtaalamu huyo maalum amesema katika ripoti yake ya mwaka  2013 kwa Baraza la Haki za Binadamu alitoa wito kwa serikali ya Marekani kutoa ripoti hii bila kuchelewa zaidi na kuhakikisha kwamba itachapishwa kikamilifu bila kuhaririwa kupita kiasi.

Aidha  Emerson amesema wakati wa kuchukua hatua ni sasa na watu waliohusika na njama za uhalifu wa wazi katika ripoti ya leo ni lazima wachukuliwe hatua ya kisheria , na wakabiliwe na adhabu inayolingana na uzito wa makosa yao.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter