Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP20 Lima iweke msingi wa mkataba wa mwakani Paris:Ban

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon akihutubia mkutano wa COP20 huko Lima,Peru. (Picha:UNFCCC)

COP20 Lima iweke msingi wa mkataba wa mwakani Paris:Ban

Nimekuja na ujumbe wa matumaini na udharura! Ndivyo alivyoanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kwenye hotuba yake kwa washiriki wa kikao cha ngazi ya juu cha mkutano wa 20 wa mabadiliko ya tabianchi, COP20 unaoendelea huko Lima, Peru.

Ban amesema inafahamika kuwa kushughulikia vitendo vya binadamu vinavyosababisha mabadiliko ya tabianchi  yasiyotakiwa ni hatua bora ya kujenga jamii zinazoweza kustahimili changamoto wakati wowote.

Hata hivyo amesema ni vyema kuchukua hatua sasa kushughulikia mambo hayo.

(Sauti ya Ban)

“Bado kuna fursa ya kuhakikisha kiwango cha joto duniani hakizidi nyuzi joto mbili za selsiyasi kilichokubaliwa kimataifa. Hata hivyo fursa  hiyo inayoyoma. Nchi zote lazima ziwe sehemu ya suluhu hii na jamii zote zishiriki. Huu siyo muda wa kucheza bali wakati wa mabadiliko.”

Katibu Mkuu ametaka maazimio ya Lima yaibuke na nyaraka bora itakayoweka msingi wa majadiliano na hatimaye maridhiano ya mkataba wa mazingira wa mwaka 2015 huko Paris.

Amesema kukabiliana kwa dhati na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu ili kuweka msingi wa maendeleo endelevu na hivyo kuepusha kupoteza mafanikio ya kiuchumi na kijamii yaliyokwishapatikana .