Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malaria yapungua Afrika, vyandarua moja ya sababu: WHO

Matumizi ya vyandarua yameleta mafanikio makubwa dhidi ya malaria. (Picha: Maktaba/Roll back Malaria)

Malaria yapungua Afrika, vyandarua moja ya sababu: WHO

Idadi ya wagonjwa wa Malaria kwenye nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara imepungua kwa asilimia 54 tangu mwaka 2000.

Hiyo ni kwa mujibu wa tathmini mpya ya ugonjwa wa Malaria kwa nchi hizo za Afrika inayoeleza kuwa hicho ni kiwango kikubwa ikizingatiwa kuwa kwenye eneo hilo ndiko kunakotokea asilimia 90 ya vifo vyote vya Malaria.

Shirika la afya duniani, WHO ambalo ndio limetoa ripoti hiyo imesema licha ya ongezeko la watu kwa asilimia 43 kwenye eneo hilo, idadi ya wale wanaougua Malaria imepungua kutoka Milioni 173 mwaka 2000 hadi Milioni 128 mwaka jana.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema sasa dunia ina vifaa sahihi dhidi ya Malaria na harakati za kinga zinafanya kazi lakini changamoto ni kuhakikisha vifaa na mbinu hizo zinafikia watu wengi zaidi ili mafanikio  yaliyopatikana yasitoweke.

Vifaa hivyo ni pamoja na vyandarua vyenye dawa na vifaa vya uchunguzi dhidi ya Malaria.

Maeneo yaliyo hatarini kupoteza mafanikio dhidi ya Malaria ni nchi za Afrika Magharibi zilizokumbwa na Ebola ambako tayari WHO imetoa mwongozo mpya wa kukabiliana na Malaria wakati wa mlipuko wa Ebola.