Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yakusanya misaada kwa wahanga wa kimbunga Hagupit

Ufilipino.(Picha ya UNICEF/HQ 2014-1959Vinas

UNICEF yakusanya misaada kwa wahanga wa kimbunga Hagupit

Huku kimbunga Hagupit kikiendelea na uharibifu nchini Ufilipino, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linachukua hatua haraka kusaidia  juhudi za dharura za serikali ya Ufilipino, kwa kutoa vifaa vya kuokoa maisha na huduma kwa watoto na wanawake katika maeneo yaliyokumbwa na mvua kubwa.

Katika taarifa, Shirika la UNICEF limesema makadirio ya hivi karibuni ya serikali yanaonyesha watu zaidi ya milioni moja wameathiriwa, hii ikiwa ni pamoja na watoto 400,000, wengi wao wakiwa katika maeneo ya uokoaji.

Kimbunga  Hagupit bado kinazidi kusonga mbele na hivyo kuleta upepo mkali wa uharibifu, mvua kubwao na kuongezeka kwa kiwango cha maji na maporomoko ya ardhi.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Ufilipino, Bi Lotta Sylwander amesema kasi ya uokoaji inayofanywa na serikali imeepusha majeruhi wengi pamoja na kuzuia vifo.

Hata hivyo, Bi Sylwander ameonya kuwa Hagupit bado ni tishio kubwa kwani maelfu ya watoto na wanawake wanahitaji misaada ya dharura, huku UNICEF na washirika wake wakifanya kazi usiku na mchana ili kukabiliana na changamoto nyingi.