Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzalishaji wa afyuni waongezeka Asia, wakulima wazidi kuwa maskini

Mmme wa afyuni.(Picha ya UNODC)

Uzalishaji wa afyuni waongezeka Asia, wakulima wazidi kuwa maskini

Uzalishaji wa afyuni huko Kusini Mashariki mwa Asia umezidi kushika kasi huku Myanmar na Laos zikiongoza kwa kilimo cha zao hilo linalotumika kutengeza madawa ya kulevya aina ya Heroin.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya ofisi ya  Umoja wa Mataifa inayohusika na udhibiti wa uhalifu na madawa, UNODC ikieleza kuwa mwaka huu afyuni kwenye nchi hizo ililimwa kwenye  jumla ya ekari 63,800 ikilinganishwa na ekari 61,200 mwaka jana.

Ripoti hiyo iitwayo utafiti wa afyuni kwa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia kwa mwaka 2014 imesema Myanmar imesalia kuongoza kwenye nchi zinazolima zaidi Afyuni ikiongeza kuwa kilimo hicho kinachofanywa na wakulima maskini  kinaendelea kutishia ulinzi, usalama na maendeleo ya ukanda huo.

Jeremy Douglas ni mwakilishi wa UNODC ukanda wa Asia Kusini na Pasifiki anaelezea madhara ya kilimo hicho.

(Sauti ya Jeremy)

“Kaya zinazolima afyuni zinapata kipato kidogo kulinganisha na wakulima wa mazao mengine, wanaishi maeneo ya ndani sana si rahisi kufikika. Afyuni pia inatengenezwa kuwa heroine na kuathiri afya za watumiaji hata nchi nyingine. Halikadhalika rushwa katika nchi kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kitokanacho na biashara hiyo na hivyo kuathiri ukanda huo.”

UNODC inachofanya sasa ni kupatia wakulima mipango mbadala ya kilimo mathalani kilimo cha Buni huko Myanmar ikisema taratibu inazaa matunda.