Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2014 ulikuwa janga kwa watoto: UNICEF

Mtoto akiwa amembeba motto mwenzake.Hapa ni kambi ya wakimbizi wa ndani huko Bambari, Jamhuri ya Afrika ya Kati. (Picha:UN/Catianne Tijerina)

Mwaka 2014 ulikuwa janga kwa watoto: UNICEF

Mwaka wa 2014 umekuwa wa vitisho, majanga na kukatisha tamaa kwa mamilioni ya watoto duniani, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wakati mwaka huu ukifikia ukingoni. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Anthony Lake amesema mwaka 2014 ulishuhudia mizozo ikizidi kushika kasi maeneo mbali mbali duniani, watoto wakilengwa kutumikishwa na vikundi vilivyojihami huku dunia nayo ikisahau majanga mengine.

Kwingineko amesema watoto wameuawa wakiwa madarasani au wamelala na wengine wakishuhudia wazazi wao wakiuawa na hivyo wao kubaki yatima.

Ametolea mfano Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Iraq na Palestina akisema takribani watoto Milioni 230 duniani kote wameathirika na majanga yanayoendelea kurindima bila kusahau mlipuko wa ebola unaotishia ustawi pia wa mtoto huko Afrika Magharibi.

UNICEF imetaka dunia ichukue hatua zaidi ili mwaka 2015 uwe wa ustawi kwa mtoto kwani kila mtoto ana haki ya kuwa na makuzi thabiti, salama na yatakayomwezesha kupata elimu kwa mustakbali wake yeye mwenyewe, jamii yake na dunia nzima kwa ujumla.