Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya ILO yabaini pengo katika usawa wa ujira

Picha@ILO

Ripoti ya ILO yabaini pengo katika usawa wa ujira

Shirika la kazi duniani ILO limezindua ripoti ya tathmini ya malipo ya mishahara duniani inayoonyesha kutokuwepo na ongezeko la ujira katika nchi zenye ustawi.

Katika uzinduzi wa ripoti hiyo mchumi wa ILO Sandra Polaski amesema maendeleo yanayoonekana kwenye malipo ya ujira ndani ya miaka miwili iliyopita ni katika nchi zinazoibuka kiuchumi kwani kwenye ukanda wa Ulaya viwango vya mshahara ni sawa na vilivyokuwa kabla ya mdororo wa kiuchumi.

Nchi za Asia kama China, Vietnam na Cambodia  zimetajwa kuchangia nusu ya ukuaji wa mishahara duniani.

Ripoti pia imebainisha pengo kubwa kati ya tija ya wafanyakazi na ujira wao ikionyesha kuwa kaya zinanufaika kidogo sana ikilinganishwa na ukuaji wa kiuchumi.

(Sauti ya Sandra)

Ni nini kinapaswa kufanywa kuhusu pengo kubwa la usawa ambalo linaibuka katika ujira, kuna baadhi ya sera hapo, kiwango ch chini cha mshahara ni moja . Nadhani kama tukiangalia historia ujira ulianza kutumika katika za nchi za Amerika Kusini kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, kama njia ya kutatua suala la usawa na nchini China miaka takriban 15 iliyopita.  China ilianza kutumia kima cha chini cha mshahara kama chombo cha kuimarisha kipato.”

Halikadhalika ILO imetaka kutokomezwa kwa sheria za ubaguzi wa kijinsia kwenye malipo ya mshahara kwani kuna tofauti ya mishahara kati ya wanawake na wanaume katika baadhi ya nchi ikitolea mfano Marekani ambako ujira wa wanawake uko chini kwa asilimia 36 ukilinganishwa na ule wa wanaume.