Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumzia uamuzi wa mahakama New York

Jiji la New York. (Picha:Rick Bajornas)

Ban azungumzia uamuzi wa mahakama New York

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametaka mamlaka zote nchini Marekani kuchukua hatua zipasazo ili kushughulikia madai ya uwajibikaji zaidi miongoni mwa maafisa wanaosimamia sheria.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric  amewaambia waandishi wa habari kuwa wanafahamu kinachoendelea jijini New York, Marekani  kufuatia uamuzi wa Jumatano wa mahakama kutomfungulia mashtaka polisi anayedaiwa kumuua mmarekani mweusi Eric Garner mwezi Julai mwaka huu.

(Sauti ya Dujarric)

“Nafikiri kisa hiki ni fursa nyingine ya kuangalia uwajibikaji wa maafisa wanaosimamia sheria. Katibu Mkuu anazisihi pande zote kushughulikia madai yanayotaka uwajibikaji zaidi. Halikadhalika anakaribisha tangazo la wizara ya sheria ya Marekani ya kufungua uchunguzi wa kiraia kwenye tukio hilo.”

Ban amesema maandamano mengi yameshuhudiwa jijini New York na Katibu Mkuu amesihi waandamanaji kufanya hivyo kwa amani huku akitaka mamlaka ziheshimu haki za waandamanaji.