Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utu na watu viwe msingi wa malengo endelevu:Ban

Sayari ya dunia (Picha-Maktaba)

Utu na watu viwe msingi wa malengo endelevu:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amelihutubia Baraza Kuu kuhusu ripoti yake inayotoa mwelekeo wa mchakato wa mjadala wa malengo ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.

Ban amesema katika mchakato wa ripoti hiyo imebainika kuwa licha ya maendeleo kupatikana katika baadhi ya maeneo bado umasikini na ukosefu wa usawa ni dhahiri duniani, wanawake na watoto pamoja na vijana bado wanaenguliwa kwenye shughuli za jamii zao. Amesema dalili za uharibifu wa mazingira na mizozo ya kijamii zimezingira dunia nzima.

Kwa mantiki hiyo amesema malengo ya maendeleo endelevu ni lazima yaweke misingi ya kuondoa mapengo yaliyodhihirika wakati wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia na utekelezaji wake ndio jaribio kuu .

“Ajenda mpya ijumuishe mambo yenye mvuto na misingi kwa kuzingatia haki za binadamu na utu. Itahitaji ahadi za dhati za kifedha na hatua nyingine za utekelezaji. Na ni lazime iwe thabiti, jumuishi kwa umma katika ngazi zote za utoaji taarifa, ufuatiliaji, mambo ya kujifunza na uwajibikaji wa pamoja.”

Kwa mantiki hiyo ametaja mambo ya kuzingatia kwenye ajenda ijayo ya maendeleo endelevu kuwa ni utu, watu, ustawi, hali ya sayari ya dunia, haki na ubia.