Chuo kikuu cha Harvard chatambua mchango wa Ban duniani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametunukiwa tuzo ya mwaka ya kibinadamu na chuo kikuu cha Harvard cha nchini Marekani kutokana na mchango wake katika masuala ya kimataifa.
Alitunukiwa tuzo hiyo Jumanne ambapo akizungumza wakati wa sherehe hiyo ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua zaidi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kutokomeza matumizi ya silaha za nyuklia, ugonjwa wa Ebola na masuala ya haki za binadamu.
Ban amesema wakati Umoja wa Mataifa unajiandaa kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake hapo mwakani, dunia inacho cha kujivunia kutokana na maendeleo yaliyopatikana tangu vita vikuu mbili za dunia zilizochochea kuanzishwa kwa chombo hicho.
Hata hivyo amesema licha ya maendeleo yaliyopatikana bado ukatili dhidi ya wanawake unatishia jamii zote, halikadhalika ubaguzi dhidi ya makundi madogo na usafirishaji haramu wa binadamu.