Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwezeshe waathirika wa mizozo dhidi ya msongo wa mawazo: Eliasson

Jan Eliasson, Picha ya UN

Tuwezeshe waathirika wa mizozo dhidi ya msongo wa mawazo: Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema katika ulimwengu uliojaa majanga na mizozo, ni muhimu kuimarisha uwezo wa watu kukabiliana na hali hizo ili kuweza kumudu mistuko na misongo ya mawazo.

Amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa sera uliondaliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA na kufanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Bwana Eliasson amesema mi muhimu kujiandaa katika kukabiliana na  majanga ikiwa yanatarajiwa na kuongeza kuwa ni muhimu jumuiya ya misaada ya kibidamu ikajipanga vyema kwa shirikiano na wale wanaofanya kazi katika masuala ya maendeleo na haki za binadamu.

Hata hivyo amesema licha ya dunia kutawaliwa na mizozo akitolea mfano ule wa Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Syria na hivyo kuathiri mamilioni ya maisha ya watu kinachomfariji ni kuwa  hatua zimepigwa katika utekelezaji wa baadhiya malengo ya maendeleo ya milenia.