Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo ya teknolojia yajumuishe watu wenye ulemavu:Ban

Teknolojia imewezesha hata vijana hawa kushiriki kwenye mashindano ya soka. (Picha:UNDESA)

Maendeleo ya teknolojia yajumuishe watu wenye ulemavu:Ban

Leo ni siku ya kimataifa ya watu wanaoishi na ulemavu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ujumbe wa mwaka huu unaolenga maendeleo endelevu na ahadi ya teknolojia kuimarisha ustawi wa kundi hilo umekuja wakati muafaka.

Ban amesema teknolojia imebadilisha ulimwengu kwa kupanua wigo wa fursa lakini bado idadi kubwa ya watu wanaoishi na ulemavu wameachwa nyuma.

Amesema teknolojia jumuishi za kisasa zinaweza kuongeza uwezo wa kundi hilo kujikwamua kwenye lindi la umaskini na hata kuwawezesha kujiokoa pindi majanga yanapoibuka.

Ban amesema jitihada zote zitumike ili sera, mipango na miongozo ya teknolojia mpya kwa karne ya 21 ijumuishe watu wenye ulemevu ili maendeleo endelevu yawe na manufaa kwa wote.