Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa makazi kusaidia wahanga wa vita huko Bosnia-Herzegovina:UNHCR

Familia inayotarajia kunufaika kwa kupata nyumba chini ya mradi wa mpango wa makazi. Picha: UNHCR/N.Lukin

Mpango wa makazi kusaidia wahanga wa vita huko Bosnia-Herzegovina:UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa kushirikiana na wadau wake wa kimataifa ikiwemo muungano wa Ulaya umeandaa mpango wa makazi kwa ajili ya makumi ya maelfu ya wananchi waliopoteza makazi yao wakati wa miongo miwili ya vita huko Bosnia-Herzegovina.

Mwakilishi mkazi wa UNHCR huko Bosnia- Herzegovina, Andrew Mayne, amesema mpango huo wa jumla ya Euore zaidi ya Milioni 100 unalenga makazi kwa ajili ya kaya 5,400.

Hata hivyo awamu ya kwanza ya mpango huo itahusisha ujenzi wa nyumba 170 zitakazogharimu takribani Euro Milioni 2.5 na kumaliza kashfa ya kihistoria ya watu kulazimishwa kukimbia makazi yao huko Bosnia-Herzegovina, Croatia, Montenegro na Serbia.

Bwana Mayne amesema baadhi ya wakazi wamesubiri usaidizi huo kwa miaka 20 akisema kuwa kuanza kwa mradi huo ni kitendo cha kihistoria na kwamba wanufaika wa kwanza watatambuliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu na ujenzi kuanza mwakani.