Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Aina mpya za utumwa ni janga kwa mamilioni duniani:ILO

Picha ya ILO/© Cao peng / Imaginechina 2014

Aina mpya za utumwa ni janga kwa mamilioni duniani:ILO

Ikiwa leo ni siku ya kumbukizi ya kumalizika kwa biashara ya utumwa ya kupitia bahari ya Atlantiki, Shirika la kazi duniani, ILO limetaka kasi zaidi iongezwe kuhakikisha aina mpya za utumwa ikiwemo utumikishaji kwenye ajira vinatokomezwa ifikapo mwishoni mwa karne hii.ILO imesema licha ya mafanikio kwenye harakati za kuondokana na vitendo hivyo, bado kazi ni kubwa kwa sababu aina mpya za utumwa zinaibuka kila uchao zikizalisha vipato vikubwa lakini machungu kwa mamilioni.

Mathalani imesema biashara hiyo ya utumikishaji kwenye ajira huzalisha faida ya dola Bilioni 150 kila mwaka duniani kote ambapo theluthi mbili ya mapato hayo hutokana na na utumikishaji wa wanawake na watoto kwenye sekta ya ukahaba na starehe.

Sekta nyingine zilizotajwa kunufaika na utumwa wa kisasa ni zile za kilimo, ujenzi, viwanda na madini ambapo ILO inasema utumikishaji umeenea nchi tajiri na maskini.

Shirika hilo limesema muarobaini wa janga hilo ni kutokomeza ajira zisizo na mifumo inayoweza kufuatiliwa pamoja na kuwapatia watu elimu na stadi za kutosha ili waondokane na umaskini.