Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msimamo dhidi ya Ebola usilegezwe:WHO

Wahudumu wanaohusika na mazishi ya waliofariki dunia kutokana na Ebola wakiwa kwenye jukumu lao nchini Liberia. (Picha: WHO/P. Desloovere)

Msimamo dhidi ya Ebola usilegezwe:WHO

Shirika la afya duniani,WHO limesema mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kutokomeza Ebola kwenye nchi tatu zilizokumbwa zaidi na ugonjwa huo uko katika mwelekeo sahihi lakini hiyo haimaanishi tayari ugonjwa huo umedhibitiwa.

Mkurugenzi msaidizi wa WHO Bruce Aylward amesema hayo mjini Geneva Uswisi alipozungumza na waandishi wa habari akionya watu wasilegeze msimamo kwani kumekuwepo na mafanikio tangu Umoja wa Mataifa utangaze mpango wake wa dhidi ya Ebola  huko Liberia, Sierra Leone na Guinea miezi miwili iliyopita.

Mpango wa Umoja wa Mataifa ujulikanao kama 70-70-60 unahusisha kuwa na asilimia 70 ya mazishi salama kwa waliofariki dunia kwa Ebola na kuhakikisha asilimia 70 ya wagonjwa wanatengwa maeneo salama ndani ya siku hizo 60.

(Sauti ya Aylward)

 “Kwa ujumla tuko mahali tofauti kabisa ikilinganishwa na siku 60 zilizopita wakati wa pengo kati ya hatua za kuchukua na ugonjwa wenyewe. Tumeona pia jamii nyingi zinabadili mwenendo wa maisha. Mara nyingi tunazungumzia idadi ya vitanda na mazishi ambayo jinsi yanavyotekelezwa yamesaidia kupunguza kasi ya mlipuko. Lakini kuna jambo linguine Tabia! Mabadiliko ya tabia huko Liberia yamekuwa ni muhimu sana.”

Licha ya mafanikio, WHO imesema changamoto iliyopo ni mgawanyiko wa kijiografia wa kuenea kwa ugonjwa huo ikitolea mfano Guinea.