Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malipo kwa wahudumu wa Ebola ni jambo la msingi na haki: UNDP

WHO/P. Desloovere )
Wahudumu wa afya wakitakasisha mavazi yao baada ya huduma. (Picha:

Malipo kwa wahudumu wa Ebola ni jambo la msingi na haki: UNDP

Shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP limesema linashirikiana na mamlaka nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone kuratibu malipo kwa maelfu ya wafanyakazi wanaotoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola.

Wafanyakazi hao ni pamoja na matabibu, wafanyakazi wa maabara, wanaofuatilia watu wanaodaiwa kuwa na Ebola pamoja na wale wanaohusika na mazishi.

Kiongozi mkuu wa UNDP Helen Clark katika taarifa yake amesema mafanikio ya kutokomeza Ebola yanategemea wanawake na wanaume hao wanaojitolea uhai wao kila uchao kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema kuwapatia malipo yao kwa wakati ni jambo muhimu na inasaidia kujikimu wao wenyewe na familia zao na vile vile kuhakikisha kuna wahudumu wa afya kila wakati ili kudhibiti mlipuko wa Ebola.

UNDP kwa kushirikiana na ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaohusika na dharura ya Ebola UNMEER kwa sasa wanafuatilia malipo na kuimarisha mfumo wa ulipaji.

Lengo siyo tu kusaidia serikali na wadau katika usimamizi na malipo ya fedha bali pia kuimarisha na kuendeleza mfumo unaoweza kurahisisha huduma za kifedha hata baada Ebola itakapotokomezwa.