Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 13 zafikia lengo la kutokomeza njaa kabla ya 2015:FAO

Mchuuzi wa mboga nchini Gambia, moja ya nchi zilizofanikiwa kufikia lengo la kupungzua njaa kwa asilimia 50. (Picha@FAO)

Nchi 13 zafikia lengo la kutokomeza njaa kabla ya 2015:FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limetambua nchi 13 duniani kuwa kwenye mwelekeo wa kutokomeza njaa hata kabla ya ukomo wa malengo ya maendeleo ya milenia hapo mwakani. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

FAO imetaja mataifa hayo kuwa ni pamoja na kutoka Afrika ambayo ni Cameroon, Ethiopia, Gabon, na Mauritius ikisema yamefikia lengo la milenia la kupunguza njaa kwa asilimia 50, halikadhalika lile la mwaka 1996 la mkutano wa dunia kuhusu chakula la kupunguza kwa kiwango hicho hicho watu wenye njaa.

Wawakilishi wa nchi hizo wamekabidhiwa vyeti maalum na Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva aliyeleza kuwa wamepitia changamoto kubwa ikiwemo mazingira duni ya uchumi na ya kisera.

Hata hivyo FAO imesema kutokomeza njaa duniani hatua zaidi zahitajika ikisema bado watu zaidi ya Milioni 800 wanakumbwa na utapiamlo uliokithiri.

Pietro Genari ni mkurugenzi wa Takwimu, FAO.

(Sauti ya Pietro)

"Mafanikio haya yanaonesha kuwa utashi wa kisiasa na uwajibikaji wa serikali na wananchi duniani  kote vinaweza kushinda njaa na utapiamlo. Kwa hiyo tuna amatumaini kwamba kwa kuonyesha mafanikio haya, FAO inatoa mwongozo na kichocheo kwa nchi nyingine  kufuata njia hiyo."

Tayari nchi 63 zinazoendelea zimefikia lengo la milenia la kupunguza njaa kwa asilimia 50 huku nyingine sita zikiwa kwenye mwelekeo huo huo.