Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuongeze kasi tutokomeze Ukimwi 2030: UNAIDS

Siku ya Ukimwi duniani 2014, punguza pengo la upimaji, huduma na matibabu kwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi. (Picha@UNAIDS)

Tuongeze kasi tutokomeze Ukimwi 2030: UNAIDS

Katika siku ya Ukimwi duniani, shirika la Umoja wa Mataifa linaloongoza harakati dhidi ya ugonjwa huo,UNAIDS limetaka hatua zaidi zichukuliwe ili kuhakikisha Ukimwi unakuwa umetokomezwa ifikapo mwaka 2030. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Sauti ya Amina)

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibe katika ujumbe wake wa siku hii amesema mafanikio yaendelea kupatikana ikiwemo kuvunja ukimya kuhusu Ukimwi, mwelekeo uliozoeleka wa maambukizi yake na hata unyanyapaa lakini hatua zaidi zinahitajika.

Amefananisha changamoto zinazokumba Ebola hivi sasa na wakati ule Ukimwi ulipoanza kwani woga na hofu vilikumba jamii huku dawa zikiwa hazipo lakini mshikamano wa kimataifa, harakati za kuelimisha jamii, mashirikia ya kiraia na wanasayansi vimeleta matumaini.

Hata hivyo amesema ni vyema kuongeza kasi ili kufikia mwaka 2020 asilimia 90 ya wanaoishi na HIV wawe wanafahamu hali zao, asilimia 90 ya hao wanaofahamu wapate matibabu na asilimia 90 ya wanaopata tiba wapunguze kiwango cha virusi.

(Sauti ya Sidibe)

“Hebu tutumie fursa ya miaka mitano ijayo tufikie ndoto yetu ya 90-90-90. Nataka kueleza dunia hii leo kuwa huu ni wakati wetu kuongeza juhudi zetu maradufu, kuongeza kasi ya vitendo vyetu, kuhakikisha tunaongeza kasi. Kwa pamoja naamini tunaweza kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.”