Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani shambulizi na mauaji Kano, Nigeria

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon. (Picha:UN/Maktaba)

Ban alaani shambulizi na mauaji Kano, Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani vikali shambulizi la kigaidi kwenye Msikiti Mkuu wa Kano, Nigeria hii leo, ambalo limeripotiwa kuwaua watu kadhaa na kuwajeruhi wanaokisiwa kuwa mamia ya wengine.

Bwana Ban ametuma rambirambi zake kwa familia za wahanga, pamoja na watu na serikali ya Nigeria, na kuwatakia majeruhi nafuu haraka.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa mamlaka za Nigeria ziwafikishie haraka waliotenda uhalifu huo mbele ya mkono wa sheria, akikariri kuwa hapawezi kuwepo kisingizio chochote kinachokubalika cha kufanya mashambulizi dhidi ya raia.

Ban ameahidi uungaji mkono kikamilifu wa Umoja wa Mataifa kwa juhudi za Nigeria za kupambana na ugaidi, na kutoa ulinzi kwa raia, kwa kuzingatia sheria ya kimataifa na wajibu wa Nigeria kuhusu haki za binadamu.