Wanajeshi wa UM nchini Mali hawakukimbia majukumu yao- MINUSMA

28 Novemba 2014

Walinda amani 30 kati ya walinda amani 170 wa kutoka Chad wa Umoja wa Mataifa hawakukimbia majukumu yao kaskazini mwa Mali kama ilivyoripotiwa katika vyombo vya habari, umesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSMA.

Mnamo Novemba 25, walinda amani hao 30 kati ya kundi la wanajeshi 170 waliokuwa kwenye kituo cha Aguelhok, karibu na mji wa Kidal, waliondoka kwenye kituo hicho wakielekea kambi nyingine ambako walikutana na kamanda mkuu kutoka Chad pamoja na naibu kamanda wa kikosi cha MINUSMA, ili kuelezea malalamishi yao kuhusiana na hali ngumu ya maisha katika kambi yao na kucheleweshwa malipo yao.

Katika mahojiano na Radio ya Umoja wa Mataifa msemaji wa MINUSMA, Radhia Achouri amesema kwamba walinda amani hao hawakukimbia majukumu yao, na hivyo inapotosha kutumia neno 'kukimbia', kama ilivyoandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari.

"Ukweli ni kwamba, askari jeshi hao 30 waliamua kulileta suala hili kwa wafanya maamuzi. Kwa hiyo, siwezi kukiita 'kuasi' na siwezi kukiita kukimbia. Bila shaka ingalikuwa bora iwapo wangechukuwa hatua tofauti, lakini hali imekuwa ilivyo. Walileta malalamishi yao kwa viongozi wa MINUSMA na viongozi wa Chad. "

Halikadhalika msemaji huyo amesema kuwa askari jeshi hao wanatarajiwa kurejea kwenye kituo chao leo Ijumaa au Jumamosi. Umoja wa Mataifa umekuwa ukiisaidia Mali kujikwamua kutoka kwenye mzozo wa kisiasa uliofuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2012.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter