Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, inakadiriwa watoto millioni 1.1 wamezuiwa kuambukizwa virusi vya ukimwi, huku visa vipya vya uambukizaji vikishuka kwa asilimia 50 kati ya mwaka 2005 na 2013.
UNICEF imetoa taarifa hiyo kabla ya Siku ya Ukimwi Duniani itakayoadhimishwa jumatatu Tarehe Mosi, Disemba, ikitaja chanzo cha mafanikio hayo kuwa kupanuliwa kwa upatikanaji wa huduma ya kuzuia uambukizaji wa mtoto kutoka kwa mama, PMTCT miongoni mwa mamilioni ya akina mama wajawazito wanaoishi na virusi vya HIV.
Huduma hiyo ni pamoja na matibabu ya Ukimwi kwa mama, ambayo yanapunguza maambukizi ya virusi kwa watoto na kuwaweka hai mama na katika hali nzuri ya afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Anthony Lake amesema kama tunaweza kuzuia visa vipya vya milioni 1.1 vya maambukizi ya Ukimwi kwa watoto, tunaweza kulinda kila mtoto kutokana na Ukimwi.