Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio la Boko Haram lawalazimu watu 3,000 kukimbilia Niger

Wakimbizi wakikimbia vurugu la Boko Haram katika mji wa Borno, Nigeria, wakitafuta makazi katika kijiji cha Guesseré, Niger. Picha: IRIN / Anna Jefferys(UN news centre).

Shambulio la Boko Haram lawalazimu watu 3,000 kukimbilia Niger

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limesema kuwa sambulizi la kundi la Boko Haram mapema wiki hii katika mji wa Damassak, kaskazini mwa Nigeria liliwaua watu 50 na kuwalazimu wengine 3,000 kukimbilia eneo la Diffa katika nchi jirani ya Niger. Taarifa kamili na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdullahi)

Wahudumu wa UNHCR huko Diffa wamesema kuwa wakimbizi bado wanawasili kutoka Nigeria kufuatia shambulizi hilo, na kwamba wakati wengi wao wakisubiri boti za kuwavusha mto wa Komadougou Yobé mpakani, baadhi yao wanajaribu kuvuka kwa kuogelea.

Wakazi wa eneo hilo wameripoti kuwa wamewaona watu wakizama na kufariki dunia wanapojaribu kuvuka mto. Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR..

“Wengine waliripotiwa kupigwa risasi na Boko Haram, ambao waliwafuata hadi kwenye ukingo wa mto. Kulingana na wale wanaowasili, wengi wa wakimbizi, hususan wanawake, watoto, wazee na majeruhi, bado wanasubiri kuvuka mto ili waingie Niger.”

Bwana Edwards amesema watoto wengi walitenganishwa na wazazi wao wakati wa shambulizi hilo, watu wakikimbilia Niger.

“Katika mji ulio karibu zaidi wa Chetimari, watoto na watu wazima wanarandaranda karibu na makazi ya muda, wakiwatafuta jamaa zao. Wakimbizi wanasema hawakuwa na muda wa kuchukua chochote, na waliacha kila kitu nyuma.”