Mauaji Beni yafikia watu 200, MONUSCO kubadili mbinu zake

26 Novemba 2014

Wakati idadi ya watu waliouawa kwenye mapigano huko Beni, jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Congo, DRC ikifikia 200, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO umesema unabadili mbinu zake za operesheni kufuatia tukio la kuviziwa wakati wakiwa doria. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.(Taarifa ya Assumpta)

Kamanda Mkuu wa vikosi vya MONUSCO, Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz ameiambia radio ya Umoja wa Mataifa kuwa tarehe 19 mwezi huu kikosi kimoja kilichokuwa doria kilishambuliwa baada ya kuviziwa na wahalifu wakati kikielekea uwanja wa ndege kutoka Beni.

(Sauti ya dos Santos Cruz)

“Bahati nzuri hatukuwa na majeruhi wowote kutoka wenzetu wa polisi. Na bado tunachunguza wahusika wa shambulio hilo.”

Hata hivyo amesema tayari wamechukua hatua..

(Sauti ya dos Santos Cruz)

Tumebadili mfumo wetu wa utendaji katika kudhibiti mwenendeo wa wahalifu na serikali tayari nayo inachunguza. Ilikuwa ni hali ambayo hatukutarajia lakini tunaimarisha uwezo wa vikosi vyetu.”

Katika hatua nyingine Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mauaji dhidi ya raia huko Beni ambako tangu yaanze katikati ya mwezi uliopita, watu wapatao 200 wameshauawa. Wajumbe wameeleza mshikamano na MONUSCO wakisema hawatavumilia jambo lolote linalokwamisha utendaji wake.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud