Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutokomeze ukatili dhidi ya wanawake na wasichana wakimbizi: Wataalamu

Wakimbizi wa CAR walioko Cameroon. (Picha@Unifeed)

Tutokomeze ukatili dhidi ya wanawake na wasichana wakimbizi: Wataalamu

Jitihada thabiti na za pamoja za kitaifa na kimataifa ni muhimu katika kuzuia na hatimaye kutokomeza ukatili na ghasia dhidi ya wanawake na wasichana wakimbizi.

Hiyo ni kauli ya Chaloka Beyani, mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wakimbizi wa ndani aliyotoa leo siku ya kimataifa ya kutokomeza vitendo vyote vya ukatili dhidi ya wanawake.

Beyani amesema wanawake na wasicahna ni karibu nusu ya wakimbizi zaidi ya Milioni 33 duniani kote waliopoteza makazi yao kutokana na vita, ghasia na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Amesema mazingira ya ukimbizini yanaongeza hatari ya kukumbwa zaidi na ukatili wa kijinsia na hivyo ni vyema hatua zichukuliwe kukabiliana na vitendo vinavyowakumba.

Naye Rashida Manjoo ambaye ni mtaalamu huru kuhusu ukatili dhidi ya wanawake amesema hata wakimbizi hao wanapohamishiwa kambini bado wanakabiliwa na ukatili kutokana na kuwepo kwa mazingira ya watekelezaji vitendo hivyo kukwepa sheria.

Ametaka hatua zaidi zichukuliwe kuwakinga wanawake na wasichaan hao siyo tu kwenye kambi bali pia kwenye jamii na kaya zao.