Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza muda wa UNMISS

UN Photo/Loey Felipe
Baraza la usalama likijadili Sudan Kusini. Picha:

Baraza la Usalama laongeza muda wa UNMISS

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja limepitisha azimio nambari 2187 (2014) la kuongeza muda wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS hadi tarehe 30 Mei mwakani. Taarifa kamili na Joseph Msami.

(Taarifa ya Joseph Msami)

Azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya UNMISS limepitishwa mara tu baada ya Baraza la Usalama kupitisha azimio lingine la kuongeza muda wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Guinea Bissau kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Disemba mosi. Akizungumza baada ya kupitishwa azimio hilo, Mwakilishi wa Kudumu wa Sudan Kusini kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Francis Deng amesema..

“Tunakaribisha kuongeza muda wa mamlaka ya UNMISS, na tungependa kushukuru kwa dhati nchi zinazochangia vikosi vya wanajeshi na polisi kwa ujumbe wa kulinda amani, licha ya mazingira magumu ambamo unafanyia majukumu yake.”

Balozi Deng pia amezungumza kuhusu wajibu wa kutatua mzozo, na ahadi ya serikali ya Sudan Kusini kuendeleza mazungumzo ya amani..

“Wajibu wa msingi wa kutatua matatizo ya Sudan Kusini, upo mikononi mwa viongozi wake. Jamii ya kimataifa inaweza kusaidia, lakini haiwezi kuleta suluhu kutoka nje. Ni kwa msingi huu, ndio serikali imejikita kwa mchakato wa amani na SPLM kinzani, tangu mapigano yalipoanza Disemba 2013.”