Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya ICT duniani yaongezeka, Denmark yaongoza

Mtandao wa mawasiliano. (Picha:ITU)

Matumizi ya ICT duniani yaongezeka, Denmark yaongoza

Zaidi ya watu Bilioni Tatu duniani wako kwenye mtandao na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano unaozidi kupata mapokeo mazuri karibu katika kila nchi.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la mawasiliano duniani, ITU iliyotolewa Jumatatu ikionyesha kuwa katika nchi zilizoendelea kiwango cha matumizi ya intaneti duniani kimeongezeka kwa asilimia 6.6.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa katika nchi zinazoendelea kiwango ni asilimia 8.7 ilhali kwa nchi zilizoendelea kiwango cha ukuaji ni asilimia 3.3.

Hata hivyo asilimia 90 ya watu Bilioni 4.3 wasiotumia intaneti wako nchi zinazoendelea ambapo ITU inasema wengi wao wako vijijini.

Katibu Mkuu wa ITU Dkt. Hamadoun I. Touré amesema ripoti hii ni muhimu katika mchakato wa kuendelea sekta ya ICT kwa kuwa ni vyema kufahamu pengo lililopo ili kuwa na mipango bora.

Ripoti hii inatambuliwa kuwa ni ya kina kwa kutoa takwimu na uchambuzi na hutumiwa na serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi duniani kote.

Ripoti imehusisha nchi 166 ambapo Denmark ni ya kwanza, Jamhuri ya Korea ni ya pili ambapo nchi za Afrika zilizopo kwenye kundi la nchi 100 ni Mauritius, Seychelles, Misri na Afrika Kusini. 

Kenya imeshika nafasi ya 124, Uganda 146, Rwanda 148 na Tanzania 152.