Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutafanya kila tuwezalo kukomesha Ebola- Ban

Picha: Morgana Wingard/ UNDP

Tutafanya kila tuwezalo kukomesha Ebola- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amewaambia waandishi wa habari mjini Washington, D.C kuwa, Umoja wa Mataifa utafanya kila uwezalo kuzisaidia nchi zilizoathiriwa na Ebola kuukomesha mlipuko wa homa hiyo, kuwatibu walioambukizwa, kuhakikisha kuwa huduma zote muhimu zinatolewa, na kutunza ustawi wa nchi na kuzuia kuenea kwa kirusi hicho katika nchi zingine.

Ban ameyasema hayo baada ya mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, ambao ulifanyika kwenye makao makuu ya Benki ya Dunia mjini Washington, D.C. Katibu Mkuu amesema, viwango vya maambukizi vinaongezeka katika maeneo mengi, na kuongeza kuwa usaidizi zaidi wa kimataifa unahitajika, ukiwemo wa timu za madaktari na wahudumu wa afya wa kujitolea, hususan katika wilaya zilizo ngumu kufikika.

“Na tunahitaji kuepukana na kupiga marufuku usafiri, ubaguzi dhidi ya wahudumu wa afya na hatua zingine ambazo zitazitenga nchi ambazo zinahitaji usaidizi zaidi. Kumekuwa na ufanisi kidogo wa kutia moyo. Pale mchakato wa kukabiliana na Ebola unapotekelezwa, viwango vya maambukizi mapya vinapungua. Tunaona mabadiliko katika maeneo mengi, na yanatupa tumaini.”

Ban amesema ufanisi huo mpya unatokana na ushirikiano wa serikali na jamii mashinani na mfumo wa Umoja wa Mataifa, watu kuchukua hatua za kujilinda, kuongezeka viwango vya mazishi salama, uwezo mkubwa zaidi wa kutibu wagonjwa, na mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa kulivalia njuga tatizo la Ebola. Hata hivyo, ameeleza kusikitishwa na hali nchini Mali…

“Msururu mpya wa maambukizi Mali unatia wasiwasi mno. Tunageuza mafunzo tuliyopata kutokana na mlipuko wa Ebola kuwa vitendo vya mapema, ili kuzuia uenezaji zaidi nchini Mali. Viongozi wa Mali wamedhihirisha uongozi mzuri na uhimili tangu mlipuko uanze. Wameomba usaidizi wa UNMEER.”

Katibu Mkuu pia ametangaza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Dr.Margaret Chan na Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS,  Dr. Michel Sidibé, wanaondoka mara moja kuelekea Mali Ijumaa mchana, kama njia ya kuonyesha mshikamano wa Umoja wa Mataifa na serikali na watu wa Mali.