ICN2 yatamaishwa, Sierra Leone yazungumzia mahitaji muhimu dhidi ya Ebola

21 Novemba 2014

Mkutano wa pili wa kimataifa wa lishe umefunga pazia huko Roma, Italia ambapo mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO Jose Graziano da Silva amesema mkutano huo umefungua njia kwa nchi kukubaliana ajenda za kutokomeza njaa na utapiamlo.

Bwana da Silva amesema anaamini muongo ujao unatakiwa utambuliwe kama muongo wa maendeleo, na kutokomeza njaa na utapiamlo.

Miongoni mwa walioshiriki mkutano huo ni Naibu Waziri wa Afya wa Sierra Leone, Foday Sawi ambaye kando mwa kikao aliieleza Radio ya Umoja wa Mataifa harakati dhidi ya Ebola ugonjwa ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu Elfu Moja nchini mwake.

 (SAUTI YA Foday Sawi)

 “Bado tunahitaji msaada. Kwa sababu, mathalan, vifaa vya kujikinga vinatumika kila siku, na  kila baada ya kuvitumia unavitupa, unavitumia, unavitupa. Bado tunahitaji magari ya kuwasafirisha wagonjwa  kutoka kwenye jamii hadi vituo vya muda halafu kwenda vituo vya matibabu, na pia tunahitaji kuwa na uwezo wa haraka wa kuwaondoa wale waliofariki dunia kutoka vituo vya matibabu hadi makaburini  ili kuwazika”

Naye Waziri wa Kilimo wa Sierra Leone Marie Jallow akazungumzia nafasi ya lishe katika vita dhidi ya Ebola.

 (SAUTI Marie Jallow)

 “Ili kufanikisha lishe nchini mwetu, hali  baada ya Ebola itakuwa muhimu sana. Na naamini mkutano huu baada ya kurejea nyumbani utatujengea nafasi kubwa ya sisi kuingiza programu za usalama wa chakula na usalama wa lishe nchini mwetu”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud